Hii ni spesho kwa wanaopenda wake za watu!
TUPO kwenye kipindi kigumu cha kupambana na Virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19. Tuzidi kuchukua tahadhari za kujilinda zinazotolewa na Serikali kama kunawa mikono kila wakati na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na zaidi ya yote tumuombe Mungu janga hili lipite!
Tukirudi kwenye darasa letu la uhusiano, leo tunazungumzia wale ambao ni mabingwa wa kupenda wake za watu. Najua wapo wake za watu wanaopenda waume za watu, lakini leo nitajikita zaidi kwa wanaume.
Najikita kwa wanaume maana najua wao ndiyo kwa kiasi kikubwa wanakuwa wa kwanza kuwarubuni wanawake. Wanatumia vishawishi vyao, wanawahadaa wake za watu na kujikuta wameingia kwenye mtego bila kujijua.
Hii inatokana na jinsi walivyo na mbinu za kushawishi. Mwanaume anamuanzia mbali sana mke wa mtu. Anajifanya kama vile hana mpango naye, anajifanya kuwa msaada. Anamshawishi kuwa rafiki wa kawaida, baadaye anatupa ndoano.
Baada ya kipindi kirefu cha urafiki kupita, kutokana na uhuru ambao mke amejipa au kupewa na mume wake, basi anajikuta ameweza kusaliti bila hata mumewe kujua. Anazoea mchezo huo na sasa ukiangalia, jambo hili limekuwa la kawaida.
Wake za watu kutembea na wanaume wengine, siyo jambo la kushangaza. Watu wanafurahia uhusiano wa nje kuliko ule wa ndani. Maisha haya ndiyo ambayo yapo kwa sasa. Wengi tu wanaishi kwa staili hii, wanawake wana waume zao, lakini wanatembea nje bila wasiwasi.
Ndugu zangu, ninyi wanawake kwanza mnapaswa kutambua kwamba, kufanya hivi ni hatari. Kuendelea kuendekeza mchezo huu si kwamba mnainjoi maisha, bali mnajidhalilisha. Ni fedheha sana kuendelea kufanya hivi, mnajiaibisha!
Ni hatari pia hata kuleta maradhi ndani ya nyumba. Mwanamke hata kama una tatizo gani na mumeo, hakikisha unalimaliza. Kama kuna kitu hakuridhishi mumeo, ni vizuri kumueleza ili aweze kubadilika. Mfanye mumeo kuwa tiba yako, kuweni huru kuelekezana jinsi ya kuridhishana.
Usihangaike kuitafuta tiba sehemu nyingine. Mume wako ndiye uliyemchagua kufanya naye maisha. Kumsaliti ni dhambi. Kumsaliti hakukupi heshima, kunavua heshima na hata jamii ikijua inakudharau. Jitahidi sana usithubutu kabisa kujaribu, itafute furaha ya ndoa kwa mumeo kadiri uwezavyo.
Nikirudi kwa wanaume ambao mnapenda hii tabia, jueni kwamba si ujanja. Kutembea na wake za watu siyo ujanja.
Ni jambo ambalo linaweza kukutokea hata wewe. Unamfanyiaje mwenzio jambo kama hilo, halafu ukajiona mjanja?
Acha kabisa kufanya jambo hilo. Wanawake wapo wengi, kwa nini utembee na mke wa mtu? Tena mbaya zaidi unafanya ukiwa unajua kabisa huyu ni mke wa fulani, si busara kabisa. Hiyo ni dhambi ambayo inaweza kukurudia.
Unayomfanyia mwenzako na wewe unaweza kuja kufanyiwa. Vuta picha utajisikiaje pindi mkeo akiwa anatembea na watu nje, halafu watu wakawa wanajua na kukudharau wewe kwamba huna uwezo au humfurahishi mkeo?
Tulia na mwanamke mmoja, ukiona mnaendana ni vizuri ukafanya uamuzi wa kuoa. Na ukioa, tulia! Achana na mambo ya kuhangaika mara huyu mara yule. Ni vizuri kutengeneza maisha, kuboresha uhusiano wako na kuijenga familia iliyo bora na salama.
Chagua kujiheshimu. Jiheshimu wewe na mwenzako aliyejitoa kuoa. Usimtongoze mke wa mtu. Tafuta wa kwako.
Kwa leo inatosha.
Comments
Post a Comment